Skip to Content

mast image
Wycliffe Bible Translators

Additional Jesus resources in Swahili:

Swahili is spoken in the following countries:

  • Tanzania
  • Kenya
  • Rwanda
  • Uganda

Yesu - Swahili

Here are some extracts from a Swahili translation of the Bible that talk about Jesus. The extracts are from the Gospel of Mark.

Get Adobe Reader to view this pdf filePDF version extracts of Mark (44kB)
PDF version whole of Mark (167kB)
You will need Adobe Reader to view pdf files, which can be downloaded free here



Mark 1.1

1. Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

Mark 1.14-15
14. Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema,
15. "Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!"

Mark 1.21-27
21. Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika Sunagogi, akaanza kufundisha.
22. Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.
23. Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu,
24. akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!"
25. Yesu akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu."
26. Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka.
27. Watu wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!"

Mark 1.32-34
32. Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo.
33. Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.
34. Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.

Mark 2.1-12
1. Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani.
2. Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,
3. wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne.
4. Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya dari iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.
5. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Mwanangu, umesamehewa dhambi zako."
6. Baadhi ya walimu wa Sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,
7. "Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake."
8. Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
9. Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu aliyepooza, Umesamehewa dhambi zako, au kumwambia, Inuka! Chukua mkeka wako utembee?
10. Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,
11. "Nakwambia simama, chukua mkeka wako uende nyumbani!"
12. Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, "Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili."

Mark 4.35-41
35. Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Tuvuke ziwa, twende ng'ambo."
36. Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Palikuwapo pia mashua nyingine hapo.
37. Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji.
38. Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, "Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?"
39. Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, "Kimya! Tulia!" Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa.
40. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?"
41. Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, "Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?"

Mark 5.22-24
22. Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake,
23. akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi."
24. Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande.

Mark 5.35-42
35. Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?"
36. Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu."
37. Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo.
38. Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi.
39. Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu."
40. Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana.
41. Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!"
42. Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi.

Mark 7.18-23
18. Naye akawaambia, "Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi,
19. kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?" (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.)
20. Akaendelea kusema, "Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi.
21. Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,
22. uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.
23. Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu najisi."

Mark 9.2-8
2. Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao,
3. mavazi yake yakang'aa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe.
4. Eliya na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu.
5. Petro akamwambia Yesu, "Mwalimu, ni vizuri sana kwamba tuko hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."
6. Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema.
7. Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, "Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni."
8. Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao.

Mark 12.28-31
28. Mmojawapo wa walimu wa Sheria alifika, akasikia mabishano yao. Alipoona kwamba Yesu aliwajibu vyema, akajitokeza akamwuliza, "Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?"
29. Yesu akamjibu, "Ya kwanza ndiyo hii: Sikiliza, Israeli! Bwana Mungu wetu ndiye peke yake Bwana.
30. Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.
31. Na ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi."

Mark 14.10-11
10. Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alienda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu.
11. Makuhani wakuu waliposikia habari hiyo, walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti Yesu.

Mark 14.44-46
44. Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: "Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni, mkampeleke chini ya ulinzi."
45. Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akasema, "Mwalimu!" Kisha akambusu.
46. Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.

Mark 15.6-15
6. Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka.
7. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji.
8. Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake.
9. Pilato akawauliza, "Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"
10. Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu.
11. Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba.
12. Pilato akawauliza tena, "Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?"
13. Watu wote wakapaaza sauti tena: "Msulubishe!"
14. Lakini Pilato akawauliza, "Kwa nini! Amefanya kosa gani?" Lakini wao wakazidi kupaaza sauti, "Msulubishe!"
15. Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe.

Mark 15.33-39
33. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa kulikuwa giza nchini kote.
34. Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eloi, Eloi, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"
35. Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, "Sikiliza! Anamwita Eliya!"
36. Mtu mmoja akakimbia, akachovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, "Hebu tuone kama Eliya atakuja kumteremsha msalabani!"
37. Yesu akapaaza sauti kubwa, akakata roho.
38. Basi, pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.
39. Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake aliona jinsi Yesu alivyolia kwa sauti na kukata roho, akasema, "Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!"

Mark 15.42-46
42. Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato.
43. Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Armathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila uoga, akaomba apewe mwili wa Yesu.
44. Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo.
45. Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu auchukue mwili wake.
46. Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango.

Mark 16.1-7
1. Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.
2. Basi, alfajiri na mapema siku ya Jumapili, jua lilipoanza kuchomoza, walienda kaburini.
3. Nao wakawa wanaambiana, "Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa kaburi?"
4. Lakini walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.)
5. Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi upande wa kulia; wakashangaa sana.
6. Lakini huyo kijana akawaambia, "Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza.
7. Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni."

Mark 16.15-16
15. Basi, akawaambia, "Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu.
16. Anayeamini na kubatizwa ataokolewa; asiyeamini atahukumiwa.

Mark 16.19-20
19. Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu.
20. Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.




Copyright information: Public Domain